0


Kipa aliyekuwa akikipiga kwenye kikosi cha Simba, Vincent Angban (pichani juu), ameibuka na kusema amesamehe kila kitu kilichotokea kwenye klabu hiyo ikiwemo madai yake baada ya kuvunjiwa mkataba.

Angban, kwenye usajili wa dirisha dogo msimu huu alisitishiwa mkataba wake uliobaki wa miezi sita ambapo aliahidiwa kulipwa mshahara wake wa mwezi mmoja baada ya makubaliano ya kuvunjwa mkataba huo.

Taarifa kutoka ndani ya Simba, zinasema Angban alitakiwa kulipwa dola 1,000 ambazo ni zaidi ya Sh milioni 2 alizokuwa akichukua kila mwezi.


Kwa mujibu wake, mpaka anaondoka nchini mwishoni mwa mwaka jana, alikuwa hajalipwa kitu, hivyo ameamua kutofuatilia wala kuzungumzia madai hayo tena.

Akizungumza kutoka kwao nchini Ivory Coast, Angban alisema: “Sipendi kuzungumzia ishu ya madai yangu na Simba baada ya mkataba kuvunjwa kwa sababu nimeamua kusamehe kila kitu, kwa sasa nimeamua kutafuta maisha sehemu nyingine na siku si nyingi nitarudi uwanjani.


“Nipo nyumbani Ivory Coast nikijifua mwenyewe, kila siku nimekuwa nikifanya mazoezi ya gym ili kujiweka sawa huku nikisikilizia timu ya kujiunga nayo kwani kwa sasa usajili bado haujafunguliwa na kuna timu zinanihitaji, dili likikamilika nitakwambia nimejiunga na timu gani."

Chanzo: CHAMPIONI

Post a Comment

 
Top