0
Beki wa kati wa Simba, Mganda, Joseph Owino.
Na Wilbert Molandi
BENCHI limetajwa ndiyo chanzo cha beki wa kati wa Simba, Mganda, Joseph Owino kuchukua maamuzi ya kurudi kwao na kuiacha timu hiyo inayoendelea na michuano ya Kombe la Mapinduzi.
Beki huyo, hivi karibuni alirejea nyumbani kwao Uganda mara baada ya kumalizika kwa mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar ambayo Simba ilifungwa bao 1-0 huku Owino akianzia benchi.
Wakati hali hiyo ikiendelea, zipo tetesi kuwa beki huyo aliyebakiza miezi sita kwenye mkataba wake, amepangwa kuondolewa kwenye usajili wa msimu ujao wa ligi kuu ili nafasi yake ichukuliwe na Mkenya, Paul Kiongera ambaye anaendelea na matibabu.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka kwa rafiki wa karibu wa beki huyo, Owino hana matatizo yoyote ya kifamilia yaliyomsababishia arejee kwao, zaidi ya kukerwa na kitendo cha yeye kuwekwa benchi.
Chanzo hicho kilisema, beki huyo alianza kuchukia kwenye mechi ya Nani Mtani Jembe dhidi ya Yanga iliyochezwa Uwanja wa Taifa na mechi kumalizika kwa Simba kushinda mabao 2-0 ambapo alianzia benchi lakini baadaye akaingia.
“Ugumu wa namba kwa Owino ulianza baada ya timu hiyo kumsajili Musheed (Juuko) katika usajili wa dirisha dogo kwa ajili ya kukiboresha kikosi hicho.“Wakati anasajiliwa beki huyo, Owino alijua atacheza pamoja naye, lakini baadaye mambo yakabadilika na nafasi yake kupangwa Isihaka (Hassani).
“Kwa mujibu wa Owino, yeye alikuwa ameshtukia kuwepo na mipango kutoka kwa mmoja wa viongozi wa juu wa timu hiyo ambaye hamtaki Owino, hivyo akaona ni vyema aondoke zake ili awapishe mabeki hao waendelee kuichezea Simba,” kilisema chanzo hicho.
Alipoulizwa Katibu Mkuu wa Simba, Stephene Ally kuhusiana na beki huyo, alisema: “Owino aliomba ruhusa baada ya kumalizika kwa mechi dhidi ya Kagera.”

Post a Comment

 
Top