KOCHA Msaidizi wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Idd Nassor Cheche, amesema kuwa wanakipanga vema kikosi hicho kuelekea mchezo ujao dhidi ya Simba ili kuifunga tena na kulinda heshima waliyoiweka Zanzibar hivi karibuni walipoichapa na kutwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi.
Azam FC inaendelea na maandalizi makali chini ya Kocha Mkuu, Aristica Cioaba na wasaidizi wake, Cheche na Kocha wa Makipa, Idd Abubakar, ambao wamekuwa wakikiweka vema kikosi hicho kuelekea mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakapofanyika Uwanja wa Uhuru Jumamosi Ijayo saa 10.00 jioni.
Cheche mara baada ya mazoezi ya leo asubuhi, ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa vijana wake wanamorali kubwa kuelekea mchezo huo na wanaomba na kutamani Jumamosi hata ingekuwa kesho kutokana na namna walivyojiandaa vilivyo.
“Hivi sasa tunaendelea na maandalizi vijana wako kambini na mazoezi wanafanya kwa nguvu zote kwa kufuata maelekezo na makosa waliyofanya katika mechi zetu zilizopita tunaendelea kuyafanyia kazi ili tubadilike kidogo na kufanya vema zaidi katika mchezo huo.
“Hali ya vijana wangu ipo vizuri, wanamorali kubwa na wanajitihada ya kufanya kitu, sisi tunatarajia mchezo utakuwa mkali na wa ushindani lakini vijana wetu watapambana hadi tone la mwisho la damu na kuhakikisha tunalinda heshima tuliyoiweka Zanzibar,” alisema.
Nafasi ya Azam kutwaa ubingwa
Akizungumzia muelekeo wa ligi ulivyo na nafasi waliyopo kama bado wako kwenye mbio za ubingwa, Cheche alisema wataendelea kupambana hadi mwisho katika kusaka taji la ligi hiyo.
“Bado tunamechi nyingi hatuwezi kusema labda tukate tamaa, lolote linaweza kutokea kwa hiyo sisi tunataka kuhakikisha mechi zetu zote zilizobakia tunashinda, kama aliyetangulia atateleza basi sisi tutachukua nafasi yake,” alisema.
Timu hizo zinakutana wakati Azam FC ikiwa nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ikibeba pointi 31 ikizidiwa pointi 14 na Simba iliyojikusanyia 45 kileleni, Yanga ni ya pili ikiwa nazo 43 huku Kagera Sugar iliyocheza mchezo mmoja zaidi ikikamata ya tatu ikiwa nazo 34.
Post a Comment