Kiungo mshambuliaji nyota wa Simba, Emmanuel Arnold Okwi.
Musa Mateja na Martha MbomaKIUNGO mshambuliaji nyota wa Simba, Emmanuel Arnold Okwi, ameshindwa kujizuia kumwaga machozi wakati akielezea tukio lake la kupigwa kiwiko ‘pepsi’ na beki Aggrey Morris kuwa ni la kikatili na lingeweza kumsababishia hata ulemavu kwa kuwa baada ya kuanguka alimmalizia kwa kumkita teke.
Okwi, raia wa Uganda, ameliambia Championi Jumatano kuwa, hakujua kama Morris angeweza kumpiga kwa kuwa hawana ugomvi na wala hawakuwa wamekorofishana siku hiyo huku akisisitiza kama ndiyo hivyo, atashindwa kuendelea kucheza Tanzania.
Okwi alianguka na kupoteza fahamu baada ya kudaiwa alipigwa na Morris katika mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar, Jumapili iliyopita na akakimbizwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Tayari uongozi wa Simba, umeonyesha picha za video kuthibitisha alipigwa.
“Ndugu yangu nazungumza tu lakini kichwa kinaniuma sana, huwezi kuamini alichonifanyia Aggrey, maana tulikuwa kwenye mchezo wa kawaida tu hakuna hata tulichojibizana labda kwa ubaya, lakini nimeshangaa sana kunipiga pepsi kichwani, tena akaona haitoshi nikiwa chini akanikita na mguu, hapo ndiyo nikapoteza fahamu kabisa.
“Naumia, najiuliza vipi anaweza kunifanyia unyama ule bila ya kosa? Nilikuwa kazini kama yeye. Sikusema neno baya, nilikuwa napambana kuipa Simba ushindi, inaniuma sana.“Nilizinduka uwanjani, lakini nilianza kujitambua vizuri nikiwa hospitali na nilipozinduka kitu cha kwanza kuuliza ilikuwa matokeo ni ngapingapi, nilipoambiwa 1-1 nikahuzunika.
Jambo hilo angefanyiwa mtu asiye na mazoezi, basi sasa hivi kungekuwa na maafa, kiukweli kama wahusika hawatashughulikia matatizo yetu ya uwanjani, ni wazi kabisa tutashindwa kucheza mpira wa Bongo na zaidi tutabaki kufanyiana fujo na kukamiana kila siku,” alisema Mganda huyo na kuongeza:
“Najua mpira siku zote huwa ni ‘fair play’, sasa alivyofanyiwa (Amissi) Tambwe na mimi leo naona kama kuna mchezo mchafu unatengenezwa kwetu (wageni). Sasa siwezi kucheza mechi dhidi ya Mbeya City, sitaweza kuungana na wenzangu kuipigania timu yangu,” alisema na kuangua kilio kwa mara nyingine.
Jana, Katibu Mkuu wa Simba, Stephene Ally, alionyesha picha za video mbele ya waandishi namna Morris alivyompiga pepsi Okwi na kueleza kwamba Simba tayari imepeleka barua TFF kutaka hatua za kinidhamu zichukuliwe kwa nahodha huyo wa Azam FC.
Wiki iliyopita, gazeti hili lilinasa picha ya mshambuliaji wa Yanga, Tambwe, raia wa Burundi, akikabwa shingoni na beki wa Ruvu Shooting, George Michael, hali iliyozua gumzo na sasa ni tukio la Okwi na Aggrey ambalo bado lina utata.
Katika mazoezi ya jana ya Simba, Dege nje kidogo ya jiji la Dar, Okwi alifanya mazoezi na wenzake lakini kila ilipofikia wakati wa mazoezi magumu alikuwa akitolewa nje na kuachwa afanye mazoezi mepesi.
Simba itavaana na Mbeya City kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, leo Jumatano.
Post a Comment