UKISEMA Arsenal ni kichwa cha mwendawazimu hutakosea maana baada ya kichapo cha mabao 5-1 katika mechi yao ya awali dhidi ya Bayern Munich kwenye michuano ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, leo tena imepokea kipigo hicho hicho kutoka timu hiyo hiyo kwenye mechi ya marudiano.
Mechi hiyo ya marudiano imepigwa kwenye Uwanja wa Emirates ambapo Arsenal ndiyo walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Theo Walcott katika dakika ya 20 ya mchezo.
Dhahama kwa upande wa Arsenal ilianza mara baada ya beki wake Laurent Koscielny kupewa kadi nyekundu baada ya kumfanyia madhambi Robert Lewandowski katika eneo la hatari na kuamuliwa ipigwe penalti.
Lewandowski ndiye aliyekwamisha kimiani penalti hiyo na kuisawazishia Bayern Munich katika dakika ya 54 na kufanya matokeo kuwa 1-1.
Baada ya pengo la Koscielny, Arsenal walianza kupoteana mbali na kuwa nyumbani na kupelekea kuruhusu mabao mengine manne kutoka kwa Arjen Robben dakika ya 68, Douglas Costa dakika ya 78, na Arturo Vidal aliyetupia mawili dakika ya 80 na 84.
Kitendo hicho kimezidi kuongeza hasira kwa mashabiki wa Arsenal waliokuwa na mabango ya kumtaka kocha wao Arsene Wenger aachie ngazi.
Kwa matokeo hayo, Arsenal wametupwa nje ya michuano hiyo kwa jumla ya mabao 10-2.
Post a Comment