BAADA ya kupata kibali cha kufanya kazi nchini juzi, Kocha Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Aristica Cioaba (pichani juu), amejinasibu ya kuwa yeye ni aina ya kocha anayependa falsafa ya soka la kushambuliaji na sio kujilinda.
Cioaba aliyesaini mkataba wa kuinoa Azam FC mwezi mmoja na nusu uliopita, wakati ilipokuwa ikishiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi na kutwaa taji hilo, ameweka wazi hayo mara baada ya jana kuiongoza timu hiyo kwa mara ya kwanza akiwa benchini katika ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Red Arrows ya Zambia.
“Mimi ni kocha ninayependa soka la kushambulia, sio aina ya kocha ninayependa timu yangu icheze kwenye eneo la kujilinda, napenda kuwapa mabao mengi mashabiki wanaokuja uwanjani kushuhudia mechi na kuwafanya baada ya mechi wawe na furaha.
“Lakini ninachoweza kukuambia hili linahitaji hatua kwa hatua mechi hadi mechi, leo ilikuwa dhidi ya Zambia (Red Arrows), hivi sasa tuna siku nne za kujiandaa kuelekea mchezo ujao (Mwadui FC) tutakaocheza hapa nyumbani (Azam Complex) na ni muhimu kucheza vizuri na kukusanya pointi zote tatu,” alisema.
Auzungumzia mchezo
Kocha huyo wa zamani wa Aduana Stars ya Ghana, alisema kuwa mchezo huo ulikuwa mzuri sana na anafuraha kubwa baada ya wachezaji wake kucheza vizuri na kwa nguvu muda wote pamoja na kupata matokeo mazuri ya ushindi.
“Ninapenda sana mechi nyingi za kimataifa za kirafiki kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya Afrika (Kombe la Shirikisho), hii ni mipango yetu ya baadaye na kila mtu ananielewa mimi, nimekuja hapa mwezi mmoja na nusu uliopita, kibali change cha kazi kimeshakamilika.
“Kwa muda huo nilianza kazi tokea nikiwa Zanzibar kabla ya mchezo wa Simba, nimekaa pamoja na benchi langu la ufundi, Babu Cheche (Kocha Msaidizi), Idd (Kocha wa Makipa), Alando (Meneja wa timu) na kila mmoja kwenye mazoezi, mashabiki walikuwa hawanioni kwenye benchi lakini kwa muda wa mwezi mmoja na nusu nilikuwa hapa kila siku katika mazoezi, hatua kwa hatua napenda timu yangu icheze mchezo mzuri na ipate matokeo mazuri,” alisema.
Alisema kuwa katika mchezo huo, timu yake ilitengeneza nafasi tatu hadi nne za kufunga mabao kipindi cha kwanza lakini hazikuweza kutumiwa vema huku akisema kuwa mambo yatabadilika baadaye na timu hiyo kuweza kufunga nafasi wanazopata.
“Inahitajika kufanya kazi kubwa, kuna baadhi ya matatizo kwenye ushambuliaji kwa baadhi ya washambuliaji, nitafanya kazi kila siku na ninawaamini wachezaji wangu watafika kiwango cha juu na hapo baadaye kuweza kufunga mabao na kila mmoja kufurahia,”alisema.
Aidha alisema kuwa anaiamini timu yake na kama ikiendelea kucheza kwa namna hii na kila mmoja kufika mazoezini na kufanya kwa nguvu na kwa umakini na kushika kile anachowafundisha na kucheza kwa kiwango kikubwa zaidi ana uhakika watachukua pointi tatu kwenye mchezo huo.
Azam FC inayodhaminiwa na kinywaji safi cha Azam Cola burudani kwa koo na mwili wako pamoja na Benki bora inayokimbiza nchini ya NMB, inatarajia kucheza dhidi ya Mwadui katika mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika Jumapili ijayo saa 1.00 usiku ndani ya Uwanja wa Azam Complex.
Credit: www.azamfc.co.tz
Post a Comment