Mogella aliyekuwa mkali wa kufumania nyavu ameyafunguka hayo leo wakati akiongea na Radio EFM kupitia kipindi cha Sports HQ ambapo ameeleza kuwa mechi za watani wa jadi kila muda unavyokwenda zinazidi kupoteza radha tofauti na ilivyokuwa enzi zao.
Mogella amesema wachezaji wengi wa sasa hawajui wanafanya nini na huenda hii inatokana na mfumo wa sasa ambapo mchezaji anasaini mkataba na baada ya hapo anakuwa analipwa mshahara wake hivyo hana sababu yoyote ya kujituma au kuongeza bidii tofauti na enzi zao ambapo wachezaji walikuwa wakilipwa kutokana na mapato ya mlangoni 'Gate Collections'.
Staa huyo aliyejiunga na Simba mwaka 1981, anaongeza kuwa, enzi zao mchezaji alikuwa anaonyesha uwezo wa hali ya juu ili aendelee kuaminiwa na timu yake ndiyo maana soka safi lilikuwa linaonekana uwanjani hasa mechi za watani wa jadi.
"Nyakati hizi mchezaji anasajiriwa miaka miwili, mwaka wa kwanza anacheza vizuri lakini msimu unaofuata kiwango kinapotea tofauti na nyakati hizo, mchezaji akiwa fiti anakuwa kweli fiti kwa takribani miaka mitano au 10" amesema Golden Boy.
Aidha mkali huyo aliyejiunga na Yanga baada ya kuachana na Simba mwaka 1992, na kuichezea kwa msimu mmoja tu kabla ya kustaafu soka mwaka 1994, amewatupia pia lawama viongozi wa vilabu vya Simba na Yanga ambao wameamua kuwaweka mbali wakongwe wake na kujifanya hawaitaji msaada wowote kutoka kwao jambo ambalo halisaidii soka letu maana wakongwe hao walikuwa na mbinu ambazo pengine kwa sasa hazitumiki.
"Vilabu hivi vimeamua kabisa kuwaweka mbali wakongwe, vinashindwa kuangalia wenzetu huko nje wanaendeshaji soka lao, hawa wakongwe wana msaada sana katika kuongeza morali na kutoa mbinu kwa vijana wa sasa hasa katika mechi hizi kubwa kama ya Simba na Yanga" Alisema staa huyo aliyekuwa na uwezo wa aina yake.
Post a Comment