0

Kuelekea mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kati ya Azam FC na Mbeya City kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam leo saa 1:00 usiku hapa chini ndiyo rekodi ya timu hizo zilipokutana.

Kihistoria tokea Mbeya City icheze kwenye ligi kwa mara ya kwanza msimu wa 2013/14, timu hizo zimekutana mara saba katika ligi hiyo, huku rekodi ikionyesha kuwa timu hiyo ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya haijawahi kuifunga Azam FC katika mchezo wowote.

Katika mechi hizo, Azam FC imeshinda mara tano na ikishuhudiwa mechi mbili zikiisha kwa sare, zote zikipigwa Uwanja wa Azam Complex huku sare ya kukumbukwa zaidi ni ile ya mabao 3-3.

Mbali na historia hiyo, itakumbukwa kuwa Aprili 13, 2014, mabingwa hao wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup) waliandika rekodi ya kutwaa taji la ligi kwa mara ya kwanza pale walipoichapa Mbeya City mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, mabao yaliyofungwa na Gaudence Mwaikimba na nahodha John Bocco ‘Adebayor’ aliyetupia la ushindi.  

Mara ya mwisho timu hizo kukutana kwenye ligi ilikuwa ni Septemba 10 mwaka jana jijini Mbeya, ambapo Azam FC ilipata ushindi wa mabao 2-1 yaliyowekwa kimiani na mawinga Khamis Mcha na Gonazo Ya Thomas, ambaye hayumo kikosini baada ya kusitishiwa mkataba, bao la Mbeya City lilifungwa kwa mkwaju wa penalti na Rafael Alpha.






Post a Comment

 
Top