MAKOCHA wasaidizi wa timu mbili zitakazoumana kesho katika fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi kati ya Simba na Azam wamezidi kutambiana kuelekea mpambano huo uliosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini.
Kwa upande wa Kocha Msaidizi wa Simba, Mganda Jackson Mayanja yeye amesema kwamba hawataki kufikishana kwenye penalti na Azam kesho.
Kikosi cha Simba SC. |
Akizungumza kwa niaba ya bosi wake, Mcameroon Joseph Marius Omog, Mayanja amesema mchezo wa kesho dhidi ya Azam utakuwa mgumu, lakini watajitahidi kuumaliza mapema siyo kufikia katika penalti kama ilivyokuwa kwa watani wao wa jadi Yanga katika mechi ya nusu fainali.
Naye Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Nassor Cheche, ameweka wazi kuwa wanajua namna ya kuikabili Simba na kupata matokeo mazuri kwenye mchezo huo wa kesho.
Kikosi cha Azam FC. |
Cheche ameongeza kuwa ni kweli mchezo utakuwa mgumu lakini wamewaona Simba tokea mwanzo wa michuano hii na mwalimu wao Omog, awali alikuwa kocha wao hivyo wanamjua vizuri na wanajua ni vitu gani watafanya hapo kesho ili kuibuka mshindi na kulitwaa Kombe la Mapinduzi.
Mechi hiyo kali itapigwa saa 2:15 usiku katika Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Post a Comment