Azam FC Inacheza Nusu Fainali Ikiwa Haijaruhusu Hata Bao Moja Ndani ya Dakika 270
KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, leo Jumanne saa 10.15 jioni itakuwa na kibarua kizito cha kusaka fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi, itakapochuana na Taifa Jang’ombe kwenye mchezo wa nusu fainali utakaofanyika Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Azam FC inaenda kucheza hatua hiyo ikiwa imeweka bonge la rekodi kwenye michuano hiyo baada ya kuwa ndio timu pekee yenye safu ngumu ya ulinzi kutokana na kutoruhusu wavu wake kuguswa ndani ya dakika 270 (sawa na mechi tatu).
Safu ya ulinzi ya Azam FC chini ya mabeki wa kati Mghana Yakubu Mohammed na Aggrey Morris, imefanya kazi kubwa sana kwenye michuano hiyo baada ya kutengeneza uelewano mkubwa na kufanya wawe kigingi kikubwa kwa washambuliaji wa timu pinzani, ambao wameshindwa kabisa kuipenya.
Azam FC itaingia hatua hiyo ikiwa na kumbukumbu ya kuifunga Yanga mabao 4-0 kwenye mchezo wake wa mwisho wa Kundi B, huku Jang’ombe nayo ikifunga pazia la Kundi A kwa kuivua ubingwa URA baada ya kuipiga bao 1-0.
Mara ya mwisho timu hizo kukutana, ilikuwa ni Julai 31 mwaka jana kwenye mchezo wa kirafiki wa maandalizi ya msimu huu, Azam FC ikishinda bao 1-0 lilifungwa na mshambuliaji aliyekuwa katika majaribio Mburundi Fuadi Ndayisenga.
Azam FC ikitinga hatua ya fainali itakayofanyika Januari 13 saa 2.15 usiku, itakutana na mshindi wa nusu fainali ya pili kati ya mechi nyingine kali ya mahasimu wa jiji la Dar es Salaam, Simba na Yanga, itakayofuatia saa 2.15 usiku.
Post a Comment