Timu za Ivory Coast na DR Congo zimeshindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 kwenye mechi yao ya pili kutoka Kundi C katika michuano ya AFCON 2017 inayoendelea nchini Gabon.
DR Congo ndiyo walikuwa wa kwanza kuliona lango la Ivory Coast kupitia kwa Neeskens Kebano dakika ya 10 ya mchezo huku straika wa Manchester City anayechezea Stoke City kwa mkopo, Wilfried Bony akiisawazishia timu yake kwenye dakika ya 26.
Dakika mbili baada ya Ivory Coast kupata bao, Junior Kabananga aliiandikia DR Congo bao la pili katika dakika ya 28 ya kipindi cha kwanza na kufanya matokeo kuwa 2-1 hadi mapumziko.
Katika dakika ya 67 ya mchezo, kiungo anayeichezea FC Basel ya Uswizi, Serey Die aliisawazishia Ivory Coast bao na kufanya matokeo kuwa 2-2.
Katika dakika za nyongeza, Solomon Kalou aliiandikia bao Ivory Coast lakini likakatiliwa na mwamuzi baada ya kuwa ameotea hivyo hadi mwisho wa mchezo matokeo yakabaki kuwa 2-2.
Baada ya matokeo hayo, Ivory Coast wamefikisha pointi 2 huku DR Congo wakiwa na pointi 4.
Post a Comment