0



 
Kiungo mshambuliaji mpya wa Simba, Hamis Kiiza.
Shaban Mbegu,Dar es Salaam
BAADA ya kuingia mkataba wa miaka miwili katika klabu yake mpya, kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Hamis Kiiza, amesema amekuja katika timu hiyo kwa ajili ya kuisaidia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Kiiza alitemwa na Yanga msimu uliopita na aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho Mbrazili, Marcio Maximo katika kipindi cha dirisha dogo baada kuonekana hafai, nafasi yake ikachukuliwa na Genilson Santana ‘Jaja’.
Lakini Simba ambao ni watani wa jadi, wameamua kumrejesha Kiiza kwenye Ligi Kuu Bara kwa kumpa mkataba wa miaka miwili.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Kiiza alisema mbali na kuja kuthibitisha ubora wake, pia ni kuhakikisha Simba inarejesha heshima yake.
Kiungo huyo mwenye kasi na kuitambua vizuri milingoti mitatu ya wapinzani, alisema kuwa atapambana kuhakikisha timu hiyo inachukua ubingwa na kucheza michuano ya kimataifa.“Kuna mambo mawili nimepanga kuyafanya nikiwa na timu yangu mpya, kwanza ni kuhakikisha naisaidia kuipa ubingwa na pili kuthibitisha ubora wangu,” alisema Kiiza.
Kiungo huyo ambaye tayari mashabiki wa Simba wamembatiza jina la Aguero, aliongeza kuwa kwa kuwa ni mzoefu katika ligi, haitampa shinda huku akitambia usajili wa timu hiyo ambao unaendelealea kufanywa.
“Hakuna kitu ambacho nilikuwa nakitamani kama kucheza timu moja na Okwi (Emmanuel), kule Uganda huwa tunakutana muda mfupi lakini sasa tutakuwa klabu moja, mashabiki wa Simba watarajie furaha tu,” alisema.

Post a Comment

 
Top