Wachezaji wa Yanga wakishangilia goli.
Sweetbert Lukonge, Hans Mloli na Wilbert MolandBEKI na nahodha Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, jana alitoa kauli ambayo inaweza kuwa shangwe kubwa kwa mashabiki wa timu yake baada ya kusema kuwa ‘anayejua anajua tu’, ikiwa ni muda mfupi baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar.
Cannavaro alitoa kauli hiyo baada ya kushuhudiwa kiungo mshambuliaji wa timu yake Mrisho Ngassa akifunga mabao mawili na kuthibitisha kuwa kiwango chake hakijafikia tamati kama wengi walivyokuwa wakisema awali.
Ngassa aliondoka katika Uwanja wa Taifa akiwa shujaa kutokana na kufunga mabao mazuri katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara dhidi ya wabishi hao wa Morogoro ambao walishindwa kabisa kujibu mapigo na kujikuta wakipata kipigo chao cha pili msimu huu.
Mabao ya Ngassa ambaye aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Kpah Sherman huku mashabiki wake wakiimba Ngassa is back, yaani Ngassa amerudi, yameiwezesha Yanga kufikisha pointi 25 na kuwa kinara katika Ligi Kuu Bara ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 22.
Akizungumzia mechi hiyo, Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm ambaye alionekana kuwa na furaha, alimsifia Ngassa kwa kuonyesha uwezo mzuri lakini akasema nyasi za uwanjani zilikuwa zikipoozesha baadhi ya matukio kutokana na mpira kutokwenda kwa kasi inayotakiwa.
Upande wa Kocha wa Mtibwa, Mecky Maxime, alisema: “Nimekubali matokeo, hakuna mchezaji wa kumlaumu, tunajipanga kwa mechi ijayo.”Ngassa ambaye alifunga mabao katika dakika ya 56 na 63 alisifiwa na kocha wake ambaye alisema anakubali kiwango chake na ndiyo maana kazi aliyomtuma aliitekeleza inavyotakiwa.
Ngassa alionekana kuleta mabadiliko muda mfupi tu baada ya kuingia akichukua nafasi ya Sherman ambaye inaonekana mpira wa Bongo umeanza kumshinda, kwani katika michezo sita ya ligi aliyocheza, hajafunga bao lolote.
Kuhusu mechi hiyo, Ngassa alifunguka: “Naamini uwezo wangu, sikuwa sawa kutokana na matatizo ya nje ya uwanja ambayo bado hayajaisha.“Matatizo ya madeni na kutolipwa mshahara kwa miezi miwili sasa, vilichangia nisiwe sawa kisaikolojia, kama nilivyosema nitapambana kuipa mafanikio timu yangu katika muda huu mfupi uliosalia wa mkataba wangu.
“Kocha aliniambia nikacheze katikati kwa kuwa mabeki wa Mtibwa ni wazito, hivyo niwaache (Simon) Msuva na (Andrey) Coutinho wawakimbize pembeni kisha mimi niingie katikati, kweli maelezo yake yakazaa matunda.”
Katika mechi hiyo washambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe na Sherman walikosa nafasi nyingi za wazi, kama timu hiyo isingepata ushindi basi hali ingekuwa tete kwao hasa kwa kuwa mashabiki wao walionekana kukerwa na hali hiyo.
Mashabiki wamvaa Ngassa
Mara baada ya mechi hiyo mashabiki wengi wa Yanga walimzunguka Ngassa ambapo walikuwa wakimpongeza huku wakipigana vikumbo katika kutaka kupiga naye picha.
Ngassa alienda kwenye gari ya Msuva aina ya Toyota Altezza akiwa na Msuva na Tegete ambaye ndiye aliyeendesha gari hilo kutoka uwanjani hapo huku umati wa mashabiki ukiwashangilia kwa nguvu.
Katika hatua nyingine, Msemaji wa Mtibwa ambaye alikuwa na tambo nyingi kabla ya mechi hiyo, Thobias Kifaru, alipotafutwa, alipozungumza alionekana kama ameikimbia mechi hiyo kwani alisema: “Sipo Dar, nipo Iringa kikazi.” Kisha akakata simu.
Post a Comment