0
VIONGOZI wa Simba kwa kauli moja walikubaliana kupitisha uamuzi wa kumtema straika Amissi Tambwe kwa kigezo cha kushuka kiwango chake, sasa mchezaji huyo yupo Yanga na Kocha Hans Van Der Pluijm amemwambia lazima ajitume awe mfungaji bora msimu huu wa Ligi Kuu Bara.
 

Pluijm aliyerejea Yanga kuchukua nafasi ya Marcio Maximo aliyesitishiwa mkataba, aliwaanzisha kwa pamoja mastrika Tambwe na Kpah Sherman katika mchezo wa juzi Jumapili dhidi ya Azam FC, lakini ni Tambwe aliyeweza kufunga bao safi la kichwa dakika ya nane akiunganisha krosi ya Salum Telela.

Kocha huyo baada ya kuridhishwa na uwezo wa Tambwe katika mchezo huo uliokuwa wa kwanza kwa mshambuliaji huyo tangu alipojiunga na Yanga Desemba 15, amempa jukumu kubwa la kuhakikisha anafunga mabao zaidi ili awe mfungaji bora kama alivyofanya msimu uliopita alipokuwa Simba ambapo alifunga msimu kwa mabao 19.

Msimu huu hadi sasa Tambwe ana mabao mawili tu katika ligi hiyo ambapo moja alifunga akiwa na Simba na jingine ndio la juzi, yupo nyuma kwa mabao matatu dhidi ya anayeongoza kwa ufungaji, Didier Kavumbagu wa Azam mwenye mabao matano.
Akizungumza na Mwanaspoti, Tambwe alisema Pluijm amemwambia ni lazima ahakikishe anatumia vizuri nafasi anazopata uwanjani kwa kufunga mabao muhimu kwa timu yake ili awe mfungaji bora tena.

“Kocha ameniambia ni lazima nihakikishe nafunga kwa kila nafasi nitakayopata ili niwe mfungaji bora, jukumu hilo tumepewa wote wawili mimi na Sherman,” alisema.
“Nimemjibu kocha kuwa nitaendelea kujituma zaidi katika kikosi chake ili niweze kutimiza alichonituma.”
Tambwe raia wa Burundi anaamini kazi yake itakuwa rahisi kwani Yanga ina viungo wengi wanaoweza kumtengenezea nafasi za kufunga kutoka pande zote za uwanja, hivyo jukumu lake ni kutafuta nafasi nzuri ya kumuwezesha kutimiza lengo lake.

AWASHTUA
PLUIJM, PHIRI
Akizungumzia uwezo ulioonyeshwa na Tambwe dhidi ya Azam, Pluijm raia wa Uholanzi alisema amefurahishwa na jinsi straika huyo alivyocheza na kuongeza Mrundi huyo hatabiriki uwanjani.
“Kwa muda aliocheza (Tambwe) kwa kweli amefanya kazi yake vizuri na kwa uwezo mkubwa, ukiangalia bao alilofunga haliwezi kufungwa na mshambuliaji ambaye hajitumi. Uzoefu ulimsaidia, kifupi Tambwe hatabiriki awapo uwanjani,” alisema Pluijm.

Kwa upande wake, Kocha wa Simba, Patrick Phiri alisema bao alilofunga Tambwe dhidi ya Azam limewaletea shida kwani amethibitisha ubora wake na hali ingekuwa mbaya kwao endapo Yanga ingeshinda.
“Tambwe ni mchezaji mzuri, naamini kufunga kwake kutaleta shida kwetu lakini ndivyo soka lilivyo, tena ni bora wametoka sare kuliko wangeshinda ingekuwa tatizo kubwa kwetu japokuwa hatupo katika nafasi nzuri kabisa,” alisema Phiri.

Post a Comment

 
Top