0
 MAMBO yakienda vizuri Simba itampa mkataba Kocha Goran Kapunovic raia wa Serbia kuchukua nafasi ya Patrick Phiri ambaye chini yake timu hiyo imeshinda mechi moja tu ya Ligi Kuu Bara katika michezo nane na ipo nafasi ya kumi.


Phiri raia wa Zambia, ameiongoza Simba katika mechi nane na kuambulia pointi tisa tu kwani imetoka sare sita na kufungwa mara moja.


Tangu Simba ilipofungwa bao 1-0 na Kagera Sugar wikiendi iliyopita, viongozi wa Simba wamekuwa katika malumbano ya muda lakini wengi wameafiki kumpa kazi Kapunovic ili kuinusuru timu na wimbi la kushuka daraja kwani hakuna dalili za kupata matokeo mazuri katika mechi za mbele.


Kapunovic amewahi kuzifundisha klabu za Polisi Rwanda na Dong Tam Long An ya Vietnam ambayo straika wa Yanga, Danny Mrwanda amewahi kuichezea.

Awali viongozi hao walikubaliana kumwondoa msaidizi wa Phiri, Seleman Matola ili nafasi yake ichukuliwe na Jean Marie Ntagwabira raia wa Rwanda ambaye ni mkurugenzi wa ufundi wa klabu ya Sunrise FC. Ntagwabira amewahi kuzifundisha Rayon FC, APR, Kiyovu FC na Atraco FC zote za Rwanda.


“Lakini leo (jana) mchana mambo yalibadilika na tumeanza mazungumzo na kocha wa Serbia ili achukue nafasi ya Phiri kwani inaonekana mambo hayataweza kubadilika haraka kama tunavyofikiri,” kilisema chanzo chetu.


Kutokana na mabadiliko hayo, Matola atapelekwa kikosi cha vijana wenye umri chini ya miaka 20 (U-20) ili akakuze vipaji vya vijana ambao wataichezea Simba baadaye lakini Phiri kama wakikubaliana taratibu za kuvunja mkataba atarudi kwao Zambia.

Moja ya sifa za kocha msaidizi, Ntagwabira ni kitendo chake cha kuiongoza APR ya Rwanda kuitoa Zamalek ya Misri katika Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2004.

Katika mchezo wa kwanza Misri, Zamalek ilishinda mabao 3-2, lakini katika marudiano jijini Kigali, Rwanda APR ilishinda mabao 4-1.


Akizungumza na Mwanaspoti kutoka Kigali, Rwanda, Ntagwabira alisema; “Ni kweli nimezungumza na watu wa Simba na wamekubali sifa zangu hivyo muda wowote tunaweza kukubaliana kuhusu maslahi kwani wamekubali kuvunja mkataba wangu wa mwaka mmoja na Sunrise.”


Hata hivyo, Ntagwabira aliipa Simba sharti la kumtumia maelezo binafsi ya kocha atakayekuwa juu yake ili kuona kama amezidiwa elimu au vinginevyo. “Siwezi kukubali kuwa chini ya kocha ambaye nimemzidi uwezo,” alisema.

Alipotajiwa kuwa atakuwa chini ya Phiri, Ntagwabira alikubali kwa kusema anamfahamu kocha huyo na yupo tayari kufanya naye kazi lakini taarifa za ujio wa kocha wa Serbia amesema atazifanyia kazi ili kujua elimu yake.

Rais wa Simba, Evans Aveva alipotafutwa alisema hana taarifa kuhusu mabadiliko hayo ya makocha lakini Mwanaspoti lina uhakika viongozi wanaoratibu zoezi hilo ni wale wanaoisaidia klabu hiyo katika mambo mbalimbali ikiwemo kuleta makocha.
Phiri tayari ameweka wazi kukubaliana na uamuzi wowote utakaochukuliwa dhidi yake na viongozi kutokana na mwenendo wa timu katika ligi.

Post a Comment

 
Top