Bata, E. Guinea
NAHODHA wa
Ivory Coast, Yaya Toure ambaye pia ni Mchezaji Bora wa Afrika, ametimiza
ndoto zake kwa kuliongoza taifa lake kutwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa
ya Afrika (Afcon) 2015 kwa kuifunga Ghana kwa penalti 9-8, usiku wa
kuamkia leo.
Ivory Coast ambayo imekuwa ikikosa kombe hilo katika dakika za mwisho
licha ya kuwa na wachezaji wengi wanaoaminika kuwa bora, imetwaa
ubingwa huo kwenye Uwanja wa Bata ikiwa ni baada ya miaka 23 kupita
kwani mara ya mwisho ilitaa mwaka 1992.
Mpaka dakika 90 za mchezo huo zinakamilika, matokeo yalikuwa 0-0,
licha ya kuongezwa dakika 30 bado timu zote zilishindwa kupata bao licha
ya kuwa kulikuwa na kosakosa nyingi hasa dakika ya mwisho.
Ghana
ndiyo iliyoanza kupata matumaini ya kutwaa ubingwa huo baada ya kupata
penalti mbili za awali huku wapinzani wao wakikosa zote.
Kibao kiligeuka na mpaka penalti tano zinakamilika kwa kila upande,
matokeo yalikuwa ni 3-3, ndipo zikaanza kupigwa mojamoja ambazo zilienda
mpaka penalti ya 11.
Kipa wa Ghana, Brimah Razak ndiye aliyekosa penalti ya mwisho kisha
mwenzake wa Ivory Coast, Boubacar Barry mwenye umri wa miaka 35 akafanya
kweli kwa kufunga. Hiyo ilikuwa ni baada ya wachezaji wote wa ndani
kupiga mikwaju hiyo na ngoma kuwa mbichi kwa kila timu.
Kabla ya mechi ya jana, mara ya mwisho Ivory Coast ilitwaa ubingwa
huo mwaka 1992 kwa kuifunga Ghana katika fainali, wakati Ghana yenyewe
ilitwaa mwaka 1982 kwa kuifunga Libya kwa penalti.
Nyota wa Ghana, Christian Atsu, ndiye aliyeibuka mchezaji bora wa michuano hiyo.
Kwingineno, Barcelona imezidi kuipumulia Real Madrid kisogoni kwenye
msimamo wa Ligi Kuu ya Hispania (La Liga) kufuatia kuifunga Athletic
Bilbao mabao 5-2 jana, huku Lionel Messi akifunga mawili. Luis Suarez
alitoa gundu kwa kufunga bao lake la kwanza La Liga. Mabao mengine
yalifungwa na Neymar na Pedro.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment