0
 

Dar es Salaam. 
Yanga imemfunga mdomo kocha wa Coastal Union,  Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ baada ya kuisambaratisha  timu yake kwa  mabao 8-0, huku mabingwa watetezi, Azam wakilazimishwa sare 1-1 na Mbeya City.

Yanga ilipata mabao yake kupitia kwa Amissi Tambwe aliyefunga   manne, Simon Msuva, mawili na Kpah Sherman, Salum Telela kila mmoja.

Hata hivyo, Sherman ndiye aliyetoa mchango mkubwa kwenye mabao ya Yanga ambako pia aliondoa nuksi kwa kufunga bao lake la kwanza la ligi katika mchezo huo uliokuwa wa upande mmoja.

Akizungumzia kipigo hicho, Julio ambaye kwa kawaida ana ‘kilimilimi’ alisema alitegemea kufungwa mchezo huo, lakini siyo mabao manane, lakini hatajiuzulu ukocha.


“Ratiba yetu inaonyesha mechi hii tulitakiwa tucheze Aprili 18, lakini juzi nikapigiwa simu kuambiwa mchezo utachezwa leo (jana) na wachezaji wangu walikuwa mapumzikoni.


“Wachezaji wangu hawakuwa na stamini, wala umakini kutokana na kutokuwa fiti kwa mchezo huu, lakini ni afadhali hali hii imetukuta na Yanga kwani kama wangekuwa Simba, tungefungwa kumi leo,” alisema Julio.

Ushindi huo umefanya Yanga kufikisha pointi 43, kileleni ikifuatiwa na  Azam yenye pointi 37 na Simba ni ya tatu na pointi zake 34.


Yanga ilianza mchezo kwa kasi na dakika ya kwanza Sherman alikosa bao akiwa yeye na kipa Bakari Fikirini kwa kushindwa kumalizia krosi ya Tambwe.


Tambwe aliwainua mashabiki kwa kufunga bao la kwanza dakika 9, akiunganisha kwa kichwa krosi ya Sherman aliyepokea mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Oscar Joshua.


Wakati Coastal ikiendelea kushanga, kinara wa  mabao Ligi Kuu, Msuva alifunga bao lake la 12 na la pili kwa Yanga katika dakika 23, baada ya kumzidi kasi beki Mfuko Abdallah.


Tambwe alipachika bao la tatu akiongezea nguvu shuti kali la umbali wa mita 25, lililopigwa na beki Juma Abdul,  dakika ya 31 na kuwafanya mabingwa hao mara 24 kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 3- 0.


Jahazi la Coastal Union liliendelea kuzama, dakika ya 48, wakati Mrundi Tambwe alipopachika bao la nne akimalizia kazi nzuri ya Msuva aliyekuwa mwiba mkali kwa ngome ya Wagosi wa Kaya.

Post a Comment

 
Top