Wachezaji wa Yanga, wakishangilia goli.
Na Sweetbert Lukonge,Dar es SalaamYANGA leo Jumamosi inacheza na Mgambo JKT katika Ligi Kuu Bara, lakini imeonyesha jeuri ya fedha kwa kumuweka katika mawindo yake beki wa kushoto Samir Nuhu ambaye Azam FC ilikuwa katika mpango mkali wa kumrudisha kundini.
Nuhu, kabla ya kuumia goti hivi karibuni na kupelekwa India kufanyiwa upasuaji, alikuwa akiitumikia Azam vizuri lakini tangu aliporejea akakosa nafasi kikosi cha kwanza na uongozi ukampangia kazi za kufanya kiwandani.
Azam ilidhani Nuhu hataweza kurejea katika ubora wake, hivyo ikafuta mpango wa kumtumia, ikaanza kumtumia Erasto Nyoni katika nafasi hiyo wakimtoa kulia ambako sasa anacheza Shomari Kapombe.
Wakati hayo yakiendelea, Yanga ilikuwa inasaka beki wa kushoto anayetumia mguu wa kushoto kwa uhalisia na ilishaanza mazungumzo na David Luhende wa Mtibwa Sugar.Lakini ghafla waliposikia sakata la Nuhu na Azam, viongozi wake wakazungumza naye na tayari amekubali kujiunga na klabu hiyo na mazungumzo yalifanyika Zanzibar wakati wa michuano ya Kombe la Mapinduzi. Mabeki wa kushoto wa Yanga kwa sasa ni Oscar Joshua na Edward Charles.
Mmoja wa viongozi wa Kamati ya Usajili ya Yanga, alisema; “Kocha ameagiza tusajili beki wa kushoto ambaye anamudu kutumia mguu wa kushoto, mwanzo tulimfikiria Luhende lakini sasa tunamsajili Nuhu yule wa Azam.”
Championi lilipozungumza na Nuhu alikiri kukubaliana kila kitu na Yanga; “Ni kweli Yanga wananitaka,
nimeshazungumza nao tangu Januari na tumekubaliana kila kitu na muda wowote nitasaini mkataba nao.”
Ili kuthibitisha ubora wake, Yanga ilimfanyia mpango Nuhu akaichezee KMKM ya Zanzibar kwenye Kombe la Mapinduzi lakini Azam ilipopata taarifa hizo ikashtuka na kumzuia beki huyo kuichezea timu hiyo ya visiwani.
Azam ilimzuia Nuhu kutoichezea KMKM na kumuahidi kumpa mkataba wa kuichezea timu yao msimu ujao lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika na mwenyewe ameamua kusajili Yanga.
Hata hivyo, habari kutoka Azam zinasema klabu hiyo ipo katika hatua za mwisho kuhakikisha Nuhu haendi Yanga ili imtumie msimu ujao katika ligi kuu kwenye beki ya kushoto kujiimarisha.
Katika kikosi cha Azam, Nyoni hutumika kama beki wa kushoto akisaidiana na Gadiel Michael na Wazir Salum ambao wote uchezaji wao unaonekana kuwa wa kawaida, hivyo kuna mpango wa kumsajili Nuhu ili kujiimarisha.
Yanga ndiyo inayoongoza ligi kuu ikiwa na pointi 34 ikifuatiwa na Azam yenye pointi 33 zote zikiwa zimecheza mechi 17.
Post a Comment